Thursday , 23rd Aug , 2018

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo taifa (CHADEMA), Freeman Mbowe amefunguka kuwa hawaogopi kwenda jela lakini wanataka wafungwe kwa haki, na kudai kuwa hawaridhishwi na mwenendo wa kesi inayowakabiri.

Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe.

Mbowe amefunguka hayo katika mkutano wake na wanahabari leo Agosti 23, 2018 ambapo amesema kuwa hawaamini katika mapambano ya ngumi, bali kwenye sheria na kuiomba mahakama itende haki dhidi ya mashtaka yanayowakabili.

Tumejitahidi kutafuta haki katika ngazi mbalimbali za Mahakama lakini bado tunaona kuna shinikizo katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuipeleka kesi hii haraka haraka”, amesema Mbowe.

Aidha ameongeza kuwa, “Hatuoni haki ikitendeka katika kesi inayoendeshwa na Hakimu Mashauri, kesi inaendeshwa kwa maelekezo ili sisi tuonekane tuna hatia, sisi hatuhusiki na mauwaji ya Akwilina, wanaohusika wao wenyewe wanawafahamu na walikuwa wanachunguza , nachotaka kusema sisi hatuogopi jela, hatuogopi kufungwa lakini tunataka tufungwe kwa haki, na kama tutahukumiwa kwa kusema kwetu acha tuhukumiwe”.

Kauli hiyo imekuja baada ya wakili Jeremiah Mtobesya aliyekuwa akiwawakilisha Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane wa chama hicho, amejitoa kwenye kesi hiyo leo Agosti 23 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Mtobesya amejitoa katika kesi hiyo baada ya Mahakama ya Hakimu Kisutu kutupilia mbali maombi yao ya kutaka kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 iahirishwe katika Mahakama ya Kisutu ili kusubiri maombi yao na rufaa yaliyowasilishwa kwenye Mahakama ya Rufani yasikilizwe kwanza na kutolewa maamuzi.