
Mbunge wa Kawe (CHADEMA) Mh. Halima Mdee.
Mdee kupitia mtandao wa twitter ameunga mkono agizo hilo huku akiwataka wananchi kujitokeza kununua samani hizo kama ambavyo Waziri Mpango aliwataka watu wenye uwezo wa kununua wajitokeze bila kuogopa chochote.
''Wenye pesa zenu mnada ukipigwa jongeeni kwa wingi. Laana ya kuku haiwezi mpata mwewe'', ni miongoni mwa maneno aliyoandika Mdee.
Dkt. Philip Mpango, Agosti 27, 2018 aliagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Paul Makonda, yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.
Tangazo la TRA lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye lilikuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, huku jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya (DICD).