Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania, mhe. Lazaro Nyalandu.
Siku mbili baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Mhe. Lazaro Nyalandu kutangaza kuifutia leseni zote za uwindaji kampuni ya Green Miles Safaris Ltd kwa makosa ya ukiukaji wa sheria ya wanyamapori, uongozi wa kampuni hiyo umeibuka hadharani na kutishia kuwa utakwenda mahakamani kupinga hatua hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, mwanasheria wa kampuni hiyo Bw. Aloyce Komba amesema hatua iliyochukuliwa na waziri Nyalandu pamoja na ile ya waziri Kivuli wa maliasili na Utalii Mchungaji Peter Msigwa zimechochewa na mbinu chafu kutoka kwa wapinzani wao kibiashara kwani hawakuwahi kupewa nafasi ya kujibu tuhuma zilizotolewa dhidi yao.
Juzi Ijumaa, waziri Nyalandu alitangaza kufuta leseni zote za uwindaji zilizotolewa kwa kampuni hiyo baada ya kuoneshwa kwa mkanda ambapo kampuni hiyo inaonekana kukiuka sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 kwa kufanya ukatili dhidi ya wanyama na kuwinda kinyume na taratibu za uwindaji.
Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, hatua ya kuifutia leseni kampuni hiyo inaenda sambamba na kuivunja idara ya wanyamapori ambayo majukumu yote yaliyokuwa chini ya idara hiyo yatakuwa chini ya mamlaka mpya ya wanyamapori itakayoundwa hivi karibuni, mamlaka aliyosema itakuwa na mamlaka kamili ya kiuendeshaji na kusimamiwa moja kwa moja na wananchi.
Jumpali iliyopita, Waziri kivuli wa maliasili na utalii Mchungaji Peter Msigwa alionesha kwa waandishi wa habari mkanda wa video na kuanika kile alichookiita kuwa ni uozo na ukiukwaji mkubwa wa sheria ya wanyama pori unaofanywa kupitia vitalu vya uwindaji.
Mchungaji Msigwa alifichua namna makampuni yaliyopewa leseni ya uwindaji ikiwemo ya Green Miles Safaris Ltd, ilivyovunja sheria ya wanyamapori kwa kuwaua wanyama wadogo, kufanya ukatili wakati wa kuwakamata na hata kukiuka sheria za kimataifa ambazo Tanzania kama nchi imeziridhia.
Aidha, Mchungaji Msigwa alimtaka waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu kuwawajibisha watendaji wote katika idara ya wanyamapori sambamba na kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni ya Green Miles Safaris ikiwa pamoja na kuifutia kampuni hiyo leseni ya uwindaji.