Monday , 15th Sep , 2014

Jumuiya ya Ulaya imeelezea kufurahishwa na muafaka uliofikiwa wiki iliyopita baina ya vyama vikuu vya siasa nchini Tanzania kuhusu mchakato wa katiba mpya.

Mkuu wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Filberto Ceriani Sebregondi.

Muafaka huo ni ule ambapo vyama hivyo vimekubaliana juu ya uundwaji wa tume huru ya uchaguzi na kuwepo kwa mgombea binafsi.

Mwakilishi wa jumuiya hiyo nchini Balozi Filberto Sebregondi, amesema hayo leo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu siku ya kimataifa ya demokrasia, ambapo amesema muafaka huo uliofikiwa baina ya vyama vya CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP na UDP, ni hatua nzuri katika kufikia ujenzi wa demokrasia ya kweli.

Balozi Sebregondi amewataka Watanzania kutambua kuwa demokrasia ni inakwenda zaidi ya ushiriki wa wananchi katika shughuli za kisiasa na uchaguzi kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakidhania na kwamba ustawi wa demokrasia ndio chimbuko la mafanikio ya kiuchumi wa taifa lolote.

Katika kuimarisha ujenzi wa demokrasia nchini, balozi Sebregondi amesema jumuiya hiyo imetoa Euro milioni tisa, zaidi ya fedha za Tanzania shilingi bilioni 18 kwa ajili ya kukuza demokrasia nchini.