Taarifa hiyo imetolewa na Kamishna kutoka Tume ya haki za binadamu na utawala bora Bwana Kelvin Mandoki, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super mix kinachorushwa na East Africa radio, na kueleza kwamba kuna wakati hata wale wanaotakiwa kusimamia usalama ndiowanaokuwa mstari wa mbele kuondoa hali ya usalama iliyopo kwa vijana.
"Vyombo vya ulinzi kuna wakati wanatumia nguvu, tume ya haki za binadamu waliliona hili na kuingilia kati na kubaini kwamba kuna mapungufu katika utendaji ndani ya jeshi la polisi, kuna watu hawajaelewa dhana ya haki za binadamu ndani ya jeshi la polisi, hivyo ikitolewa elimu ya kina jamii itapata kufahamu haki zao ni zipi ili iweze kuwa salama", alisema Bwn. Mandoki.
Bwn. Mandoki amesema iwapo serikali itaweka msingi mzuri wa elimu juu ya haki za binadamu na utawala bora, vijana watatambua umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu na usalama wao, na hatimae kuwa na taifa salama
Pamoja na hayo Bwn. Mandoki amesema pia serikali ijayo iweke bajeti ya kutosha ili kuweza kuboresha sekta za ulinzi nchini, na kuleta uadilifu kwa wafanyakazi wake akitolea mfano jeshi la Polisi, kitendo kitakachopunguza ukiukwaji wa haki za binadamu kunakotekelezwa na baadhi ya wafanyakazi wa sekta hiyo.




