Monday , 14th Jul , 2014

Utoaji wa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za awali na za msingi, imetajwa kuwa moja ya njia zitakazosaidia kuwepo kwa matumizi bora ya barabara pamoja na kupunguza ukubwa wa tatizo la ajali za barabarani nchini Tanzania.

Afisa mwandamizi wa asasi inayojishughulisha na masuala ya usalama barabarani ya AMEND Bw. Peter Amos.

Afisa Mwandamizi kutoka asasi ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya usalama barabarani ya AMEND Bw. Peter Amos, amesema hayo katika mahojiano na East Africa Radio na kufafanua kuwa hatua hiyo itasaidia kujenga kizazi kinachochukia ajali za barabarani na chenye utamaduni na ustaarabu wa matumizi bora ya barabara.

Katika kutambua umuhimu wa elimu ya awali ya usalama barabarani, Bw. Amos amesema kuwa taasisi hiyo inaendesha programu ya elimu ya usalama barabarani kwa shule za msingi ambapo mpaka sasa jumla ya wanafunzi laki moja na elfu ishirini wameshafundishwa dhana ya matumizi bora ya barabara pamoja na sheria za usalama barabarani.

Kwa mujibu wa Amos, programu hiyo inatolewa kwa msaada na kikosi cha usalama barabarani ambapo wanafunzi hufundishwa namna ya kutumia na kutambu alama za msingi za barabarani kwa lengo la kuwaepusha na ajali.