Mkuu wa Mkoa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa jiji la Dar es salaam kwa ajili ya kumpongeza Rais Dkt. Magufuli kwa kutimiza siku 100 madarakani huku akitekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Ameongeza kuwa katika shule ya msingi Maji Matitu jijini Dar es salaam imeweza kuandikisha wanafunzi 1,022 wa darasa la kwanza na kuvunja rekodi ya shule zote hapa nchini, pia shule hiyo moja ina wanafunzi 5,823 jambo ambalo kwa mujibu wa viwango vya elimu kwa idadi hiyo ya wanafunzi hao wanatosha kuanzisha shule 6.
Kwa kutambua upungufu uliopo katika shule hiyo kuanzia siku ya Jumatatu serikali kupitia mkoa wa Dar es salaam itajenga madarasa 10 katika shule ya Majimatitu wilayani Temeke.
Pia Mkoa utajenga madarasa 500 katika manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke ili kuhimili kishindo cha wanafunzi walioandikishwa.
Aidha mkuu wa mkoa amewataka watanzania wote kumuunga mkono Rais Magufuli katika utumishi wake na kuepuka kumkatisha tamaa kwani nchi inayojengwa ni moja na hakuna haja ya kugombea fito.





