Katika Mkutano huo Viongozi hao wamepanga kupiga Marufuku ya uingizwaji wa nguo za mtiumba ikiwa ni moja ya hatua zilizopendekezwa ilikuinua viwanda vya nguo katika kanda ya Afrika Mashariki ili kuondoa kabisa biashara ya uagizaji wa nguo kuukuu, maarufu kama mitumba, katika nchi hizo katika miaka michachache ijayo.
Serikali za Afrika Mashariki zimekuwa zikilaumu uagizaji wa nguo na viatu vilivyotumika kama moja ya sababu zinazofanya viwanda vya nguo na ngozi kusambaratika na hivyo kuwanyima wenyeji nafasi ya ajira.
Akizungumzia kuhusu maendeleo ya jumuiya hiyo, Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Dk. Richard Sezibera, amesema kuwa jumiya hiyo inasonga mbele kwani itifaki mbalimbali zimepitishwa kuanzia ushirikiano katika soko la pamoja, ushuru wa forodha na sasa wanaelekea kufikia hatua ya Afrika Mashariki kuwa na sarafu moja itakayotumika katika nchi zote wanachama.
Aidha katika hatua nyingine Viongozi hao pia watajadili pendekezo la kupunguza kiasi cha magari yaliyotumika yanayoingizwa ndani ya Jumiya ya Afrika Mashariki,(EAC) ikiwa ni Lengo la kutafuta mbinu ya kusaidia viwanda vya utengenezaji magari vinavyoendesha biashara Afrika Mashariki.