Sunday , 20th Dec , 2015

Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemwagiza Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga kuanza kushughulikia mgogoro wa Burundi.

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda na Mambo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga.

Huu utakuwa mtihani wa kwanza kwa Balozi Mahiga ambaye aliapishwa hivi karibuni kwenye wadhifa huo baada ya kuteuliwa na Rais kuwa mbunge. Balozi Mahiga amewaambia waandishi wa habari kuwa, ameagizwa kushughulikia kiini cha mzozo wa Burundi na tayari wakati wowote alitarajiwa kuwasili Bujumbura kuanza mazungumzo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda na Mambo ya Jumuioya ya Afrika Mashariki, alitarajiwa kuwasili kwanza mjini Arusha kwa ajili ya majadiliano na Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera na baadaye kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kushughulikia mzozo huo. Kwa sasa Tanzania ndiye mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Wakati Tanzania ikianzisha juhudi mpya kuhusiana na mzozo huo, kuna ripoti kuwa Umoja wa Afrika (AU) umeanza kujadili uwezekano wa kutumwa jeshi la Afrika Mashariki huko nchini Burundi kwa lengo la kuzima ghasia na machafuko yanayotishia kuitumbukiza nchi hiyo kwenye vita vya ndani.

Jumuiya mbalimbali za kieneo na kimataifa zimeendelea kutoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi endapo hakutachukuliwa hatua za haraka za kuhitimisha mgogoro wa nchi hiyo.