Tuesday , 29th Sep , 2015

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli amewaahidi wakazi wa Mkoa wa Iringa kuwatatulia kero mbalimbali ikiwemo kuanzisha kiwanda cha kusindika mbogamboga, kutatua kero ya maji pamoja na kuboresha sekta ya Afya.

Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na Wananchi wa Iringa

Akizungumza kwa nyakati tofauti na Wakazi hao katika mikutano yake ya Ilula, Kalenga pamoja na Iringa Mjini Mh. Magufuli amesema moja ya mikakati yake na ya Chama cha Mapinduzi ni kuboresha Sekta ya Afya kwa kiasi Kikubwa.

Mh. Magufuli ameongeza kuwa wataboresha bima ya afya ili kila mwananchi aweze kupata matibabu kwa wakati na kwa uwiano sawa tofauti na ilivyo sasa ambapo hata dawa wakati mwingine wanaambiwa wakanunue madukani ya watu Binafsi.

Aidha Mh. Magufuli amefafanua madhila yaliyompata wakati wa Uwaziri wake akiwa anawatumikia Watanzania ikiwemo kulala site za ujenzi wa madaraja na kuumwa na mbu pamoja na kuanguka kwenye helkopta jijini Dar es salaam wakati wa mafuriko.

Mgombea huyo ameongeza kuwa yeye ni mtu anayechukua sana rushwa hivyo wafanyakazi wanaofanyakazi kwa mazoea basi waanze kubadilika sasa kabla ya kuingia madarakani kwa kuwa hatawavumilia watendaji wabovu hata kidogo.

Kwa upande wake waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi amewataka wale watendaji wanauza au kunyang'anya viwanja vya watu kwa ujanja ujanja basi kiama chao ni pindi Dkt. John Magufuli atakapoingia madarakani.