Thursday , 26th Feb , 2015

Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kwa mara nyingine leo limeshindwa kumuhoji Mbunge wa Bariadi Magharibi kupitia CCM Andrew Chenge.

Baraza hilo limeshindwa kumuhoji baada ya mbunge huyo kutangaza kukata rufaa dhidi ya ombi lililotupiliwa mbali la pingamizi la zuio la Mahakama Kuu, kwa mamlaka zozote kujadili au kulifanyia kazi suala la sakata la akaunti ya Tegeta –Escrow.

Akiongea mara baada ya Hatua hiyo Mwenyekiti wa tume ya maadili nchini Jaji Hamis Msumi amesema Mhe. Chenge ameomba kukata rufaa akidai wanasheria hawajapitia vifungu vya sheria vinavyokataza kuzungumziwa kwa suala la akaunti ya Tegeta Escrow.

Kwa upande mwingine, Baraza hilo limemuhoji mbunge wa Muleba Kusini Prof Anna Tibaijuka kuhusiana na sakata hilo ambapo imeelezwa mbunge huyo alikiuka kifungu cha 12 cha sheria za maadili ya viongozi wa umma kwa kujipatia manufaa ya kifedha na kusaidia mtu mwingine kujipatia fedha.