Friday , 24th Jul , 2015

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Mtwara kimeshindwa kupata wagombea ubunge katika jimbo la Mtwara mjini na wa viti maalum kutokana na kuvurugika kwa mkutano baada ya kutokea mkanganyiko juu ya idadi ya kata zilizofanya uchaguzi.

Mmoja ya watangaza nia ya kugombea Ubunge kuptia chama cha CHADEMA mkoa Mtwara Bw, Joel Nnanauka.

Hatua hiyo ilitokana na hoja iliyotolewa na mjumbe wa mkutano huo ambaye ni mwenyekiti wa mawasiliano, takwimu na Biometric Voters Registration (BVR), Karim Salum Ally, ambaye alihoji utofauti wa idadi ya kata hizo ambapo zingine zinaonyesha ni 15 na nyingine 17.

Mwenyekiti wa wagombea kanda ya kusini ambaye ndiye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Casto Mmuni, amesema sababu iliyopelekea kuvunjwa kwa mkutano huo ni kutokana na wagombea wenyewe hawakuwa tayari uchaguzi uendelee.

Amesema baada ya kuona hakuna usawa baina yao licha ya kwamba baadaye mgombea mmoja ambaye ni Joel Nanauka kukubali ziondolewe ili uchaguzi uendelee, aliamua kuahirisha mkutano mpaka utakapoitishwa tena pamoja na kwamba mwisho wa mchakato huo wa kuchagua wagombea ni Julai 25 mwaka huu.