
Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mwitta Waitara.
Uamuzi huo wa CHADEMA umetangazwa leo Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Ukonga Omary Sweya ambapo amesema Diwani huyo alituhumiwa kwa makosa ya kutoshiriki vikao mbalimbali vya chama hicho, pamoja na kutosimamia sera za chama chake.
"Kwa niaba ya kamati tendaji ya jimbo iliyoketi kikao Januari 5, napenda kuwataarifu kwamba kuanzia sasa ninapozungumza, Dorcus Lukiko si mwanachama wa Chadema, tunatoa tahadhari kuwa kazi zozote zitakazofanywa na yeye, CHADEMA isihusishwe kwa namna yoyote ile," amesema
"Ameonekana pia baada ya uchaguzi mdogo akimzunguka maeneo mbalimbali na aliyekuwa mgombea wa CCM (Mwita wa Waitara), kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushindi alioupata bila kujali hujuma alizopata mgombea wetu na chama kwa ujumla," amesema Sweya.
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwaka 2018 katika Jimbo la Ukonga CHADEMA ilishindwa kutetea Jimbo lake baada ya kumsimamisha Mgombea wake Asia Msangi ambaye alilalamikia kufanyika kwa hujuma malimbali.