Friday , 10th Jul , 2015

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na maamuzi yaliyofikiwa na vikao mbalimbali vya maamuzi ndani ya chama hicho kuwa si za kweli kwani ratiba kamili ya vikao vya maamuzi vinaanza rasmi leo.

Katibu wa Itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema kuwa vikao vya maamuzi vya chama hicho vinaanza kukutana rasmi leo na hivyo kukanusha taarifa mbalimbali zilizosambazwa na mitandao ya kijamii kuhusiana na vikao hivyo kuwa si za kweli.

Amesema kuwa vikao vya leo vitatanguliwa na kikao cha kamati ya maadili, ambacho kitafuatiwa na kikao cha kamati kuu ambacho kitatoa majina ya watu watano ambao watakwenda kujadiliwa kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM ambacho kitatoa
majina ya watu watatu ambayo yatapelekwa kwenye mkutano mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika kesho mjini hapa.

Mkutano mkuu huo ndiyo utakaotoa jina moja la mgombea urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi.