Monday , 20th Jun , 2016

Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Vunjo James Mbatia amesema kwamba Chama cha Mapinduzi kinajaribu kuwafunga midomo jambo ambalo hawatakubaliana nazo hata kidogo.

Mbatia ameyasema hayo baada ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge leo baada ya kuanza kwa mkutano wa Bunge ambao umeongozwa na Naibu Spika Tulia Ackson Mwansasu ambapo wametoka nje wakiwa wamefunga midomo kwa karatasi na kuzishikilia kwa plasta.

''Wabunge wa CCM wanatutukana bungeni , na wanajiona bora kuliko wengine na kitendo chao cha kutaka kutuziba midomo ili zidumu fikra za mtu mmoja, hatutakubali mhimili mwingine upore mamlaka ya Bunge na hata mwalimu Nyerere alifikia mahali akakataa hoja ya zidumu fikra za mwenyekiti akimaanisha ni lazima ziwe sahihi''-amesema Mbatia.

Wakitufunga midomo ndani nje hawatatufunga kwa maana mikutano waliyokataza tutaifanya kwa kuwa ipo kisheria na wanaheshimu utu wa mwanadamu na haki ya kusema jambo mradi hawavunji sheria ya nchi.

Aidha Mbatia akizungumza kwa niaba ya wapizani amesema kwamba wabunge wa upinzani hawatashiriki kuipitisha bajeti kwa kuwa serikali haijaheshimu meza ya majadiliano ambayo ndiyo ingeweza kutoa suluhu baina ya pande hizo kwa kuwa hawakushiriki kuijadili.