Wanafunzi zaidi ya 40 wa shule ya sekondari ya mtakatifu Petro, inayomilikiwa na kanisa la Anglikana, eneo la Lwanzari manispaa ya Tabora, wamenusurika kufa baada ya Bweni wanamolala kuteketea kwa moto na vifaa vya wanafunzi, wakati wao wakiwa katika ibada.
Akizungumza na EATV kwa masikitiko juu ya tukio hilo, askofu mkuu wa kanisa hilo mhashamu Elias Chakupewa, amesema kuwa, baada ya kutokea kwa moto walipeleka taarifa kwa kikosi cha kuzima moto lakini bila kujali akaambiwa magali yote ni mabovu.
Aidha katika hatua nyingine askofu huyo amesema kuwa, kitendo cha kikosi hicho cha Zimamoto kuwa na magali mabovu wakati mji unapanuka, matumizi ya kodi za wananchi nini faida yake kama yanatokea majanga wakati hakuna jinsi ya kuwasaidia walipakodi.
Mkuu wa shule hiyo Bw. Simon Kyalla amesema kuwa, moto huo umewaathiri wanafunzi kwani wakati huu ni wa kuelekea katika mitihani, lakini uongozi utajitahidi kuhakikisha wanafunzi hao wanafanya maandalizi kwa amani na utulivu, ambapo baadhi ya wahanga wamesema kuwa wamefilisiwa na moto.
Akijibu tuhuma za kutofika katika tukio hilo Mrakibu Mwandamizi Mkuu wa Zimamoto Mkoa wa Tabora Kondo Mwamed amekiri kuwa na gali moja likiwa bovu na juhudi za matengenezo zikiendelea, ambapo Meya wa manispaa ya Tabora Mhe. Gulam Dewiji akithibitisha gari hilo kuharibika kwa zaidi ya miezi miwili sasa.