
Akitoa hoja ya kuridhiwa kanuni hizo Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Prof. Costa Mahalu, aliwaomba wajumbe wa bunge maalum la Katiba kuridhia kupitishwa kwa kanuni hizo isipokuwa vifungu hivyo namba 37 na 38.
Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo Pandu Amer Kificho aliwaongoza wajumbe kupigia kura kanuni hizo kwa utaratibu wa kupaza sauti za ndio na sio, ambapo sauti za waliosema ndio zilikuwa nyingi ikilinganishwa na waliosema sio.
Baada ya kupitishwa kwa kanuni hizo Kificho alitangaza utaratibu wa kuchagua Mwenyekiti wa Muda na baadae Makamu Mwenyekiti, ambapo utaratibu utakuwa iwapo Mwenyekiti akitoka Bara Makamu mwenyekiti atatoka Visiwani, na iwapo Mwenyekiti atakuwa mwanaume Makamu wake atakuwa mwanamke kwa mujibu wa Kanuni.
Bunge hilo limehairisha vikao vyake hadi kesho saa kumi jioni ili kutoa muda kwa wagombea Uenyekiti wa bunge hilo kuchukua fomu za uchaguzi, na wajumbe kuzisoma na kuzielewa kanuni za uendeshwaji wa bunge hilo.