Thursday , 14th Jul , 2016

Wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi imeitaka bodi ya usajili wa wataalamu wa mipango miji kuwachukulia hatua maofisa wa mipango miji wanaofanya kazi za sekta binafsi licha yakuwa wao niwaajiriwa wa serikali.

Akiongea katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa tatu wa bodi ya usajili wa wataalam wa mipango miji katibu mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Yamungu Kayandabila amesema tabia ya wataalamu hao inaipotezea serikali mapato ya kodi ya ardhi.

Dkt Yamungu amesema kuwa mbali na kuwachukulia hatua wataalam hao pia  ameitaka bodi hiyo kuhakikisha inakomesha vitendo vinavyofanywa na baadhi ya taasisi za umma zikiwemo halmashauri na sekta binafsi wanatumia makampuni yasiyosajiliwa kupima ardhi.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya usajili wa wataalam wa mipango miji Profesa Wilbard Kombe amesema kuwa mpaka sasa bodi imeanza kuhamasisha wananchi  kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za upangaji miji ili kuepuka ujenzi holela na migogoro ya ardhi.