Thursday , 24th Sep , 2015

Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Gharib Bilal awaongoza waisilamu nchini Tanzania kuadhimisha sikukuu ya Eid iliyofanyika kitaifa mjini Musoma mkoani Mara.

Mohamed Gharib Bilal

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh Dk Mohamed Gharib Bilal leo ameongoza ibaada ya kitaifa ya Eid El Hajji mjini Musoma Mkoani Mara katika viwanja vya shule ya msingi Mkendo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na waumini wa kislamu ambapo amewataka watanzania kudumisha amani wakati taifa likielekea uchaguzi mkuu.

Katika Ibaada hiyo Naibu Mufti mkuu wa Tanzania Shekh HAMIDU MASOUD JONGO amesema uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu kamwe usitumike kama chanzo cha kuleta mifarakano na kusababisha machafuko ambayo yanaweza kuhatarisha amani nchini.

Amesema machafuko yanayotokana na mifarakano ya kisiasa yamekuwa yakiyagharimu mataifa mengi duniani hivyo watanzania hawana budi kulinda amani ya nchi kwa hali na mali sambamba na kuhimalisha umoja wao hasa wakati huu taifa linapoelekea katika uchaguzi wa viongozi wake.

Amewataka wanasiasa kuacha siasa za kutumia nguvu na lugha za kutafuta ushindi kwa lazima kwani amesema mara nyingi lugha kama hizo zimekuwa zikichochea vita na ambavyo vimekuwa vikinufaisha mataisha ya nje kwa kupata sehemu ya kufanya biashara ya kuuza silaha zao.

Jijini Dar es salaam Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Suleiman Kova ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ibaada ya Eid El Hajji iliyofanyika kwenye msikiti mkuu wa Bakwata Kinondoni amewataka watanzania kudumisha na kulinda amani hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu na wakati wa kuhesabu kura hadi kuapishwa kwa Rais mpya wa awamu ya tano.