Thursday , 26th Nov , 2015

Bandari ya Dar es Salaam imetajwa kuongoza kwenye orodha ya takwimu za maeneo yanayotumika kuingiza kemikali nchini kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia januari mwaka huu.

Sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam

Akizungumza jana jijini Dar es salaam mkemia mkuu wa serikali Prof. Samuel Manyele alisema kiasi cha tani 281, 468 kati ya 472,393 zimerekodiwa kuingizwa nchini kupitia bandari hiyo.

Prof. Manyele alisema licha ya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na sheria maalum ya kusimamia na kudhibiti kemikali maeneo ya viwandani na majumbani lakini kiasi hicho cha kemikali ni kikubwa na hivyo nguvu za ziada zinahitajika ili kudhibiti hali hiyo.

Aidha Prof. Manyele ameongeza kuwa ofisi yake imeongeza idadi ya watumishi wa wakala wa maabara katika mipaka inayoingiza kemikali kwa wingi ili kuimarisha na kulinda afya za watu na mazingira katika mipaka hiyo.

Kwa upande mwingne, Prof. Manyele amesema bandari ya Dar es salaam imekuwa ikiingiza kemikali nyingi hali inayohitaji udhibiti mkubwa huku mipaka ya Tunduma, Kasumulu,Kasanga na Rusumo ikiwa mipaka inayosafirisha kemikali nyingi kwenda nchi za jirani.