Thursday , 12th Nov , 2015

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bw. Ban Ki Moon

Katika Salamu zake hizo Bw. Ban amesema uchaguzi wa mwaka 2015 ni uthibitisho wa wazi na dhamira ya muda mrefu ya Watanzania kwa demokrasia, amani na utulivu huku akisema kuwa ana imani kuwa masuala ya uchaguzi yaliyobakia yatashughulikiwa kupitia taratibu za kisheria zilizopo kwa njia ya amani na uwazi.

Bw. Ban Ki Moon amesema anaamini kuwa, chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli, serikali ya Tanzania itashughulika na juhudi za kuondoa umaskini, kuimarisha utawala bora na kuendeleza juhudi za Tanzania katika kupigania amani na utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki na nje zaidi ya ukanda huu.

Aidha Katibu Mkuu huyo amesema amewahakikishia watanzania kuwa umoja wa mataifa utaendelea kumuunga mkono Dkt. Magufuli pamoja na Serikali yake katika juhudi hizi atakazozifanya.

Katibu Mkuu Bw. Ban Ki Moon pia ameipongeza Tanzania kwa kuwa mwenza imara na wa kutumainiwa na umoja wa mataifa kwa miongo yote.

“Nathamini ushirikiano uliopo baina ya Umoja wa Mataifa na nchi yako na katika kuendeleza malengo ya UN, nakutakia mafanikio katika kutekeleza shughuli zako”. Bw. Ban Ki Moon amesema katika salamu zake