Monday , 13th Feb , 2017

Mtu mmoja mwanaume ambaye hakufahamika jina, ameauwa kwa tuhuma za wizi wa mlango, katika mtaa wa Mahina – Kanyerere Kata ya Butimba Wilayani Nyamagana jijini Mwanza  

Ahmed Msangi - RPC Mwanza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP Ahmed Msangi amesema kuwa tukio hilo limetokea tarehe 13.02.2017 majira ya saa saa 8:45 ambapo mtu huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 hadi 30, aliuawa kwa kupigwa mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufariki dunia na kundi la watu waliojichukulia sheria mkononi kwa tuhuma ya wizi wa mlango wa mbao mali ya Filbert Nkwelo.

Inadaiwa kuwa marehemu alivunja dirisha la wavu la nyumba ya Filbert Nkwelo na kuingia ndani na kuiba mlango kisha wakati anatoka nje ili aondoke watu/wananchi walimuona na kuanza kupiga yowe ya mwizi ambapo kundi kubwa la watu wakiwa na mawe na fimbo lilimvamia na kumpiga sehemu mbalimbali  hadi kufariki dunia.

Taarifa hiyo ya polisi imesema kuwa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na kifo hicho na kwamba askari wanaendelea na upelelezi pamoja na uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo