Thursday , 15th May , 2014

Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojishughulisha na haki za wanawake na watoto nchini Tanzania, yameutaka umoja wa Afrika kuingilia kati kuwezesha kuachiwa kwa wanafunzi zaidi ya 200 waliotekwa nchini Nigeria na kikundi cha Boko Haram.

Baadhi ya wasichana waliotekwa nyara na wapiganaji wa kundi la Kiislamu la Boko Haram, kutoka jimbo la Kaskazini Mashariki la Borno.

Wakitoa tamko lao la pamoja leo mara baada ya Maandamano mafupi yaliyofanyika ndani ya viwanja vya mtandao wa jinsia TGNP wanaharakati hao kutoka mashirika mbalimbali ya haki za wanawake na watoto, wameelezea kusikitishwa kwao na Umoja wa Afrika kukaa kimya na kutoonesha jitihada zozote zinazoweza kusaidia wanafunzi hao waliotekwa kuachiwa huru.

Akisoma tamko la pamoja kwa niaba ya mashirika hayo,Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Bi. Lilian Liundi amesema licha ya nchi ya Marekani kuingilia kati sakata hilo lakini Umoja wa Afrika nao una nafasi ya kuhakikisha unaunganisha nguvu za pamoja ili kuwaokoa wasichana hao na kurudi katika familia zao.