Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi la Polisi CP Paul Chagonja
Akitoa taarifa rasmi ya jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa jeshi la Polisi CP Paul Chagonja aliyelazimika kusafiri kwa helkpta kutoka Dar es salaam kwenda Tanga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema kuwa si tukio kubwa kama linavyoelezwa na baadhi ya watu na kwamba waliohusika ni majambazi na siyo magaidi.
Amesema kilichotokea ni oparesheni ya kawaida iliyofanywa na jeshi la polisi kuwasaka watu wanaosadikiwa kuwa majambazi waliodaiwa kujificha katika mapango hayo na ndipo yalipotokea mapigano hayo yaliyoambatana na kurushiana risasi na kupelekea askari hao kujeruhiwa.
Amesema baada ya hali kuwa tete, jeshi hilo lililazimu kuomba msaada kutoka kwa askari wa jeshi la wananchi Tanzania JWTZ ambao walifika katika eneo la tukio na kufanikiwa kutuliza hali ya taharuki iliyokuwa imetanda katika eneo hilo.
Kamishna Chagonja amesema askari waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga ya Bombo, na kwamba jeshi hilo linaendelea na msako ambapo hadi sasa hakuna alikamatwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda ambao ni watu wanaoishi maeneo ya jirani na mapigano hayo pamoja na mwanahabari wetu, wamesema kuwa mapigano hayo yaliyoanza jana usiku na kuendelea hadi usiku kucha na kwamba mwanajeshi mmoja wa JWTZ anahofiwa kuuawa na mwili wake umepelekwa katika hospitali hiyo ya Bombo.
Alipoulizwa kuhusiana na madai ya kuwepo kwa kifo cha mwanajeshi mmoja, CP Paul Chagonja amesema kuwa Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kutoa taarifa inayohusu wanajeshi wa JWTZ, na kuwataka wanahabari waulizie suala hilo kwa msemaji wa JWTZ.
EATV imemtafuta msemaji wa JWTZ Meja Joseph Masanja ambaye amesema kuwa si jukumu lake kutoa taarifa yoyote kuhusiana na tukio hilo, kwa kuwa tukio hilo ni la kipolisi na siyo la kijeshi.
“Ukitaka kujua taarifa yoyote kuhusu tukio hilo waulize polisi, kwa kuwa hilo ni tukio la kipolisi, sisi huku hatuna taarifa yoyote” amesema Meja Masanja.
Mwanahabari wetu alipotaka kupata taarifa zaidi kutoka katika hospitali ya Bombo ameambiwa kuwa polisi imewazuia kutoa taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.
Alipojaribu kumuuliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga Said Magalula kuhusu kifo cha mwanajeshi mmoja, Mkuu huyo wa mkoa alikiri kupata taarifa za kifo hicho bila kueleza zaidi.