Wednesday , 1st Mar , 2017

Utafiti umebaini kuwa asilimia 84 ya wananchi wanaoishi vijijini nchini Tanzania wanakabiriwa na uhaba mkubwa wa chakula ikilinganishwa na asilimia 64 ya wakazi wa mijini walioripoti kuwepo kwa tatizo hilo la chakula

Akiwasilisha matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Bwana Aidan Eyakuze amesema utafiti huo kuhusiana na upungufu wa chakula Tanzania umehusisha wananchi 1800 wa Tanzania Bara na Zanzibar kati ya tarehe 14 hadi 26 mwezi Septemba mwaka 2016 na wahojiwa 1610 kati ya tarehe 9 na 15 mwezi wa pili 2017.

Kwa mujibu wa utafiti huo wananchi wengi waliohojiwa, kati ya mwezi Septemba 2016 na Februai 2017 wamedai kuwa uhakika wa kupata chakula umepungua ambapo asilimia 78 ya wananchi wamekiri kuwepo kwa uhaba wa chakula huku asilimia 65 ya wananchi wakiwa na hofu ya kaya zao kukosa chakula cha kutosha ikilinganishwa na asilimia 45 waliosema hivyo mwezi Septemba 2016.

Aidan Eyakuze - Mkurugenzi Twaweza

Mwezi Februari 2017, asilimia 51 ya wananchi waliripoti kwamba kuna wakati hawakuwa na chakula cha kutosha kwa ajili ya kaya zao kwa muda wa miezi 3 iliyopita na asilimia 35 wakiripoti kuwa na mwanakaya mmoja aliyeshinda njaa kwa siku nzima kwa kukosa chakula.

Upungufu na uhaba wa chakula unaoendelea ni kielelezo cha hali ngumu ya maisha iliyopo na umasikini wa kipato ambapo jumla ya watu nane kati ya kumi sawa na asilimia 80 wameripoti kwamba kaya zao hazina kipato cha kutosha kukidhi mahitaji yao ya kila siku.