Asilimia 25 ya nafasi za kujiunga na elimu ya juu katika vyuo mbalimbali nchini Tanzania zimebaki wazi baada ya kukosa wanafunzi wa kujiunga na vyuo hivyo katika mwaka wa masomo 2015/2016.
Hayo yamebainika katika ripoti iliyozinduliwa leo na Taasisi ya Haki Elimu iliyoangazia mafanikio na changamoto za elimu katika serikali ya awamu ya nne na kubaini kuongezeka kwa idadi ya vyuo vya elimu ya juu huku elimu ya sekondari ikishindwa kutoa wanafunzi wenye sifa za kujiunga na vyuo hivyo.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo amesema kumekuwa na ongezeko la vyuo vya elimu ya juu kutoka vyuo 26 hadi kufikia 52 pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo hivyo kutoka 96,000 hadi kufikia wanafunzi 500,000 kwa mwaka licha ya kuporomoka kwa ubora wa elimu nchini.