Tuesday , 28th Jul , 2015

Wakala wa mbegu za kilimo ASA wametakiwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika na udhibiti wa mbegu nchini kuhakikisha wanabaini na kudhibiti uigizaji holela wa mbegu za kilimo nchini ili kuepusha wakulima kununua mbegu zisizo na ubora.

Mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Dkt. Rajab Rutengwe akiwahutubia.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Rutengwe ameyasema hayo mjini Morogoro wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa wakala wa mbegu za kilimo.

Rutengwe amesema ASA, ina wajibu wa kuhakikisha inazalisha mbegu za kutosha na zenye ubora zitakazokidhi mahitaji ya wakulima na kuwataka kuweka mipango madhubuti ya kuhakikisha wakulima wanapata mbegu katika misimu yote ya kilimo.

Naye mkurugenzi wa wakala wa mbegu za kilimo Firmin Mizambwa na katibu wa TUGHE mkoa wa ilala Gaudensi Kalyango wamesema ASA tayari inafanya kila mbinu kuelimisha wananchi kuhakikisha wanatambua mbegu zisizo na ubora na kuhamasisha wananchi kutumia mbegu zilizothibitishwa na mamlaka husika ili kusaidia wakulima wanazalisha mazao mengi na kufikia malengo ya taifa.