Monday , 5th Jan , 2015

Mwanamke mmoja  mkazi  wa  kata  ya  Buhare katika manispaa ya Musoma mkoani Mara Bi Helena Paulo mwenye umri wa  miaka 20 amejifungua watoto  wawili   mapacha ambao  wameungana katika eneo  la  kifua  hadi  tumboni.

watoto mapacha walioungana

Tukio hilo  limevuta  mamia  ya  wananchi  ambao  wamefika  katika  hospitali  ya  rufaa  mkoa  wa mara  mjini  musoma  kwa lengo  la  kutaka  kushuhudia tukio  hilo.
 
Akizungumza  na  EATV katika  wodi   ya   wazazi  katika  hospitali   hiyo  ya  rufaa ya  mkoa  wa  Mara mjini  Musoma,  muuguzi  wa  zamu  Bi  Naabu Geraruma, amesema  kuwa  mwanamke huyo  amefanikwa kujifungua  usiku   wa  saa  Saba  kwa  njia   ya  Operesheni  watoto hao   wawili  wenye  jinsi   ya  kike  huku   wakiwa  na   uzito  wa  kilo 4.6.
 
Hata hivyo  muuguzi  huyo   wa  zamu  amesema tukio  hilo  ni  la kwanza  kutokea  katika  hospitali  ya  mkoa   wa  Mara  na  kwamba   hali   za  mwanamke huyo  na watoto  zinaendelea  vema  na  taratibu  za  kumpeleka  hospitali   ya  rufaa   ya   Bugando  jijini Mwanza zimekamika.
 
Taarifa  ambazo  zimeifikia  EATV  baadaye   kutoka  jijini   Mwanza  na kuthibitishwa  na  mkurugenzi  wa  utawala na  rasmali  watu   wa  hospitali   ya  rufaa  ya  Bugando  Bi  Leah  Kagine   zinasema tayari  mwanamke  huyo   na  watoto  wamefikishwa  katika hospitali  ya  rufaa  kwa  ajili  ya  matibabu  na  uchunguzi  zaidi.