Friday , 7th Nov , 2014

Watu 12 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi na treni katika makutano ya reli eneo la Kiberege, wilayani Kilombero Mkoani Morogoro nchini Tanzania.

Treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia,(TAZARA).

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Leonard Paul amesema ajali hiyo ilitokea jana saa Tisa Alasiri ikihusisha basi aina ya Scania namba T725 na treni ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA.

Kamanda Paul amesema Jeshi la Polisi linamtafuta Dreva wa basi hilo ambaye hakufahamika mara moja na kuwa ndiye sababu ya ajali kwa uzembe wa kutoangalia alama za barabarani wakati anavuka makutano hayo ya reli na barabara.

Kamanda Paul amesema watu wote 12 waliokufa papo hapo ni abiria wa basi kati ya hao sita ni wanaume, wanawake wawili na watoto wawili wenye umri wa miaka mitano hadi sita na majeruhi walipelekwa katika hosptali ya rufaa ya Mtakatifu Fransis ya Mjini Ifakara.

Wakati huo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mheshimiwa Dkt.Joel Bendera kuomboleza vifo vya watu 12 waliofariki papo hapo na wengine zaidi ya 40 kujeruhiwa kutokana na ajali ya barabarani.

“Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa za vifo vya watu 12 waliopoteza maisha papo hapo na kusababisha simanzi kubwa kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki zao, huku Taifa likipoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo yake kutokana na ajali za barabarani”, amesema Rais Kikwete katika Salamu zake.

“Naomba upokee Salamu zangu za Rambirambi kutokana na ajali hiyo, na kupitia kwako, Salamu za Rambirambi na pole nyingi ziwafikie wafiwa wote kwa kupotelewa ghafla na wapendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema azipokee na kuzilaza Roho za Marehemu wote mahala pema peponi, Amina”, amezidi kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Amewaomba wote waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo wawe na moyo wa uvumilivu na subira wakati huu mgumu kwao wanapo omboleza vifo vya wapendwa wao. Nawahakikishia kuwa binafsi niko pamoja nao katika maombolezo hayo.

Aidha, Rais Kikwete amesema anawaombea kwa Mwenyezi Mungu watu wote waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo wapone haraka, ili waungane tena na ndugu, jamaa na marafiki zao.