Thursday , 25th Jun , 2015

Aina mpya ya utalii imebuniwa nchini ambapo sasa watalii kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kupata fursa ya kukimbia katika maeneo ya asili ikiwa ni njia tofauti na awali ambapo iliwalazimu wageni kuvitembelea vivutio kwa kutumia magari.

Mratibu wa Safari ambayo ni aina mpya ya utalii kutoka Kampuni ya Utalii ya Congema Costantine Malembela.

Kundi la kwanza la watalii ambalo linawajumuisha wageni kutoka nchi za Ufaransa, Uholanzi, Sweden na Uswisi limeanza safari yake ya takribani kilometa 125 kutoka eneo la King'ori nje kidogo ya Jiji la Arusha likifanya aina hiyo mpya ya utalii kwa kupita kandokando mwa mlima Kilimanjaro na Meru pamoja na kuzungukia katika moja ya Pori la Jumuiya ya Wanyamapori WMA Longido.

Mratibu wa Safari hiyo kutoka Kampuni ya Utalii ya Congema Costantine Malembela amekiambia kituo hiki kwamba kutokana na kuongezeka kwa ushindani katika biashara ya utalii duniani, ubunifu wa huduma hiyo mpya utasaidia kuiongezea nchi mapato yatokanayo na fedha za kigeni, ambapo watalii wameonekana kuvutiwa na fursa ya kujionea vivutio kwa ukaribu zaidi.

Baadhi ya wageni wanaojumuisha kundi la watu hamsini ambao wameianza safari ya siku tano kutembelea vivutio katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania kupitia aina mpya ya utalii wa kukimbia wamesema mvuto ulionao mlima Kilimanjaro ndio kichocheo kilichowafanya kuhamasika ili kujionea maajabu mengine yanayopatikana kandokando mwa mlima huo mrefu zaidi Afrika.

Takwimu zinaonesha kwamba Utalii ndiyo sekta inayoongoza katika kuchangia pato la Taifa hadi sasa lakini mbali ya uwepo wa hifadhi za wanyama ambazo zimekuwa zikivuta maelfu ya watalii nchini, utambulisho wa utalii wa kitamaduni nao umekuwa ukipigiwa debe na wadau wa sekta hii wakizishawishi mamlaka husika kuupa uzito unaostahili.