Wednesday , 29th Aug , 2018

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza vyombo vya usalama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwalimu anayetuhumiwa kumpiga na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Kibeta, mkoani Kagera Siperius Eradius. 

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako

Akizungumza leo Agosti 29, 2018, kwenye kipindi cha East Africa Drive, Ndalichako ameeleza kusikitishwa na tukio hilo na Serikali itahakikisha anapata adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria huku akiweka wazi kuwa hawatamfumbia macho yeyote atakayebainika kuhatarisha usalama wa wanafunzi shuleni.

Pia Profesa Ndalichako ameomba radhi kwa kilichotokea na kusema mwalimu aliyesababisha mauaji hayo hakutumwa na mtu isipokuwa utashi wake. Aidha amewaomba wananchi kuwa watulivu wakati vyombo vya usalama vinafanya kazi yake na tukio hilo lisitoe tafsiri kuwa shule  siyo mahali salama kwa watoto.

''Shule ni sehemu ambayo ni salama kwa hiyo asitokee mtu akafanya vitendo ambavyo hata wazazi wasite kuruhusu mtoto kwenda shule au asiende lakini serikali itachukua hatua kwa mtu yeyote atakayefanya shule ionekane si mahali salama'', ameeleza.

Mwanafunzi Siperius mwenye miaka 13 anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na mwalimu akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.