Friday , 5th Jun , 2015

Nchi zinazoendelea katika bara la Afrika ikiwemo Tanzania zina wajibu wa kuhakikisha kwamba taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini ili kuepukana na majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yemeelezwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya hewa nchini Dkt. Ladislaus Chang'a wakati wa mkutano wa pamoja uliowashirikisha wananchi wa maeneo ya vijijini, wakuu wa wilaya, na madiwani kutoka maeneo mbali mbali ya nchi.

Dkt. Chang'a amesema matukio mengi yanayotokana na majanga kwa mfano mafuriko na ukame yamekuwa yakitokea kutokana na wengi wa wananchi hasa wa vijijini kutopata kwa usahihi taarifa za mamlaka ya hali ya hewa.

Amesema changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa zinahitaji msukumo katika ufuatiliaji na juhudi kubwa zinatakiwa kuendelea katika kusambaza na kutumia takwimu za taarifa ya hali ya hewa ili kuweza kuchangia na kuokoa maisha ya watu na mali zao kutokana na majanga hayo ya hali ya hewa.