Utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini umebaini zaidi ya asilimia 9 ya watanzania wenye umri wa miaka 20 na kuendelea wanasumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza ya Kisukari.
Akifungua semina na upimaji wa sukari kwa wabunge na wafanyakazi wa ofisi ya Bunge, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid amesema mchango wa magonjwa yasiyoambukiza katika magonjwa yote imeongezeka kutoka asilimia 10 hadi 30 mwaka huu na kuwaomba wabunge kufanya mazoezi mara kwa mara kuzingatia vyakula wanavyoshauriwa ili kukabiliana na tatizo hilo.
Awali wenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya huduma za jamii Mh. Margaret Sitta amesema watanzania wanashtuka wanaposikia maradhi kama UKIMWI na Ebola kutokana na kutisha lakini wanasahau kuna maradhi mengine kama Sukari, Shinikizo la Damu, Saratani yanaendelea kusababisha vifo vya watanzania wengi zaidi kila siku.
Novemba 14 ni siku ya maradhi ya sukari Duniani ambapo tafiti za ugonjwa huo zimeonesha ifikapo mwaka 2035 kutakuwa na wagonjwa milioni 592 Duniani kote ambapo katika Bara la Afrika kutakuwa na wagonjwa milioni 41.4 na nusu ya wagonjwa hao watakuwa hawajaanza matibabu.
Kwa sasa asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari wanaishi katika nchi zinazoendelelea ikiwemo Tanzania.