Wednesday , 13th Jan , 2016

Takriban watu 14 wameuawa katika shambulio la bomu nje ya kituo cha kutoa chanjo ya ugonjwa wa kupooza (polio) katika mji wa Kusini Magharibi wa Quetta nchini Pakistani, kwa mujibu wa maafisa.

Wengi miongoni mwa waliouawa wanadhaniwa kuwa ni polisi waliokuwa wakilinda kliniki. Polisi wenye silaha huwalinda wahudumu wa afya wanaotoa chanjo ya kupooza nchini Pakistani ambao wamekuwa wakilengwa na mashambulio mabaya ya Islamic State miaka ya hivi karibuni.

Wanamgambo wa Islamic State wanapinga chanjo ya kupooza, wakisema ni mpango wa nchi za Magharibi wa kufunga uzazi dhidi ya watoto wa Pakistani.

Pakistan na Afghanistan ni nchi pekee zilizosalia zenye matukio mengi ya maradhi ya kupooza.

waziri katika jimbo la Balochistan ambalo Quetta ni mji mkuu wake, Sarfaraz Bugti, amesema kuwa mlipuko wa bomu hilo ulitokea mapema asubuhi wakati wahudumu wa kutoa chanjo na maafisa wa usalama walipokuwa wakiripoti kazini kabla ya kuelekea nje kwa mizunguko ya kutoa chanjo hiyo .

Polisi katika eneo hilo wanasema kuwa mlipuko huo uliwaua polisi 12, mwanajeshi mmoja na raia mmoja. Watu wapao 20 wamejeruhiwa.

Chanzo BBC