
Mtoto aliyefanikiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Muhimbili.
Akizungumza na East Africa radio leo, Daktari bingwa wa upasuaji watoto katika Taasisi ya Jakaya Kikwete, Muhimbili Dkt. Godwin Godfrey Sharao amesema kuwa endapo madaktari hasa walioko mikoani watafanya uchunguzi wa kina pindi mtoto anapozaliwa wataweza kupata watoto wengi zaidi wanaohitaji matibabu, hivyo kusaidia kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.
Aidha daktari huyo amesema kuwa uhaba wa wataalamu ambao ni madaktari bingwa wa kuchunguza magonjwa ya moyo kwa watoto nchini Tanzania ni kati ya sababu inayofanya watoto wengi nchini kufariki bila kugundulika kama alikuwa akikabiliwa na matatizo hayo.
Amesema Tanzania kuna wataalam watatu pekee waliobobea katika taaluma ya magonjwa ya watoto hali inayofanya kushindwa kuwafikia wagonjwa wengi kama inavyotakiwa.
Dkt. Sharao amesema tatizo la Magonjwa ya moyo kwa watoto ni kubwa nchini lakini linakumbana na changamoto hiyo ya watalaamu hasa vijijini hivyo serikali haina budi kusomesha madaktari wengi zaidi katika sekta hiyo ili kuokoa maisha ya watoto nchini.