Tajiri mkubwa kuliko wote katika Afrika na mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji barani, Bwana Aliko Dangote amemwambia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kuwa ujenzi wa kiwanda cha saruji kikubwa kuliko vyote Tanzania unakamilika na kuwa Rais ataombwa kukifungua Agosti mwaka huu.
Bwana Dangote, raia wa Nigeria, alikutana na Rais Kikwete, Alhamisi, Aprili 30, 2015, Ikulu, mjini Dar es Salaam ambako tajiri huyo alikuwa amekuja kumweleza Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho kinachojengwa mjini Mtwara.
“Nimekuja kukujulisha Mheshimiwa Rais kuwa kazi yetu inakwenda vizuri na tutaanza uzalishaji wa saruji kwenye kiwanda chetu mjini Mtwara kuanzia Agosti mwaka huu, katika muda wa miezi miwili hivi ijayo. Wakati huo tutakuwa tayari kukuomba uje kutufungulia kiwanda chetu hiki,” Bwana Dangote alimwambia Rais Kikwete ambaye naye amekubali kufungua kiwanda.
Kiwanda hicho cha saruji kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi kuliko kingine cha saruji chochote nchini. Kwa kuanzia kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka, kiwango ambacho ni sawa na saruji inayozalishwa sasa na viwanda vyote vya sasa nchini.Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni tano kwa mwaka.
Baada ya kuwa amesikiliza, Rais Kikwete alimwuliza Bwana Dangote: “Je tunakuhudumia vizuri katika uwekezaji wako? Nini zaidi unataka tukufanyie?”
Bwana Dangote alisema kuwa bado shughuli zao zinakabiliwa na changamoto katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupata mawe ya mkaa kutoka Kiwanda cha Makaa ya Mawe cha Ngaka, mkoani Ruvuma, upatikanaji wa uhakika zaidi wa gesiasilia kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji wa madini aina ya gypsum kwa ajili ya uzalishaji.
Rais Kikwete ametoa maelekezo ya jinsi ya kutatua changamoto hizo kwa maofisa mbali mbali wa Serikali ambao walihudhuria mazungumzo hayo, akimwahidi mwekezaji huyo kuwa Serikali yake itahakikisha inatatua matatizo yote hayo, ili kukiwezesha kiwanda kuanza uzalishaji.