Jumatano , 17th Dec , 2025

Waliojeruhiwa ni pamoja na abiria wa Coaster, wanafunzi wawili, mlinzi wa SGA na dereva wa Canter. 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limesema uchunguzi wa awali umebaini kwamba ajali ya barabarani iliyotokea Disemba 16, 2025 majira ya saa 12:15 Jioni katika eneo la Karasa, Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, kwenye Barabara Kuu ya Mbeya -Tunduma ilikuwa ni uzembe wa dareva wa gari namba T260DST, aliyegonga Pikipiki iliyokuwa mbele yake, kisha kupoteza uelekeo na kugongana uso kwa uso na gari T835DTX hali ambayo imetajwa na jeshi hilo kuchangiwa na mwendo kasi katika eneo la makazi ya watu.

Kupitia taarifa ya jeshi hilo ambalo imetolewa usiku wa kuamkia leo Disemba 17, 2025 imeeleza kwamba watu watano wamefariki dunia kutokana na ajali hiyo, wakiwemo Askari Polisi wawili wa Polisi Mkoa wa Mbeya, na watu tisa walijeruhiwa na kupelekwa hospitali kwa matibabu.

Aidha, taarifa ya jeshi la Polisi imewaorodhesha waliyofariki dunia kuwa ni H.7042 CPL Chirungu Misango John, WP.15582 PC Amina Japhari Hamisi, wote wakiwa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia Mkoa wa Mbeya. Wengine ni Adam Ibrahim Mrtin (38) Dereva wa gari T835DTX Toyota Coaster, Mkazi wa Mbeya, Dereva Pikipiki T546 DAZ Fekon ambaye bado hajafahamika na mwanamume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25-29.

Waliojeruhiwa ni pamoja na abiria wa Coaster, wanafunzi wawili, mlinzi wa SGA na dereva wa Canter.