Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji anatarajiwa kuwasili wilayani Hanang kwa ajili ya kukagua athari za moto ulioteketeza sehemu ya Hifadhi ya Mazingira asili ya Mlima Hanang, moto ambao umedumu kwa siku tatu toka Desemba 3, 2025.
Moto Mkubwa ulioanza Disemba 3 mwaka huu ambao haujajulikana chanzo chake umezuka katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mlima Hanang' ulioko mkoani Manyara. Kwa mujibu wa Ofisa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Abubakary Mpapa, moto huo uloanza Desemba 3 mwaka huu, umeharibu zaidi ya hekta 170.
Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Emmanuel Kiabo, amesema jitihada za kuuzima moto huo zinaendelea, ili kuzuia kusambaa kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu jirani na mlima.
Wakati chanzo cha moto huo kikihusishwa na shughuli za kibinadamu, hasa urinaji asali kwa kutumia moto, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga, ametoa wito kwa wananchi kuepuka shughuli zinazoweza kuharibu mlima, ikiwemo kurina asali kwa kutumia moto na uvutaji wa sigara.

