Kongamano hilo limefanyika Dar es salaam Tanzania kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) na kujaribu kutafuta suluhu ya mzozo mjini Goma, mashariki mwa DRC.
Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wameuteka mji wa mashariki wa Goma, wamekuwa wakikabiliana vikali na majeshi ya serikali ya DRC.
Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya miili 2,000, ilipatikana imetapakaa mjini Goma wiki jana kufuatia makabiliano baina ya M23 na wanajeshi wa serikali.
Kongamano la viongozi wa SADC na EAC linafanyika huku kukiwa na changamoto ya kuwaleta wadau wote wa mzozo wa DRC.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi, akiapa kutozungumza na waasi wa M23, huku EAC ikipendekeza majadiliano kati ya wote wanaohusika kwenye mzozo huo.
Katika hatua nyingine Rais Afrika Kusini ameapa kuwa atawaondoa wanajeshi wake waliopo DRC baada ya wanajeshi 14 kuuawa katika mzozo unaoendelea
Rais Ramaphosa alitoa hotuba kwa taifa usiku wa kuamkia leo
Akizungumza kuhusu uwepo wa wanajeshi wa Afrika kusini katika Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo Rais Cyril Ramaphosa, alisema watafanya kazi "ili wanajeshi wetu wanarudi nyumbani".
Katika hotuba yake kwa taifa jana usiku, Ramaphosa - ambaye amekuwa akikabiliwa na shinikizo kubwa nchini mwake kwa siku kadhaa baada ya wanajeshi 14 wa nchi yake kuuawa katika mapigano katika wiki za hivi karibuni DRC- alisema suluhu la amani lazima lipatikane.
Afrika Kusini imetuma zaidi ya wanajeshi 1,000 katika kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusaidia jeshi la DRC kupambana na waasi wa M23.