Kiongozi wa waasi ambaye wapiganaji wake wameiteka Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ameapa kuendelea na mashambulizi hadi mji mkuu, Kinshasa.
Corneille Nangaa, ambaye anaongoza muungano wa makundi ya waasi ambayo yanajumuisha M23, alisema lengo lao kuu ni kupindua serikali ya Rais Félix Tshisekedi. Taarifa zinasema waasi hao kwa sasa wanasonga mbele kuelekea Bukavu, jiji la pili kwa ukubwa katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini, licha ya wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano.
Katika hotuba ya televisheni baada ya kupoteza mji wa Goma, Tshisekedi alisema "mwitikio wa nguvu na ulioratibiwa" ulikuwa unaendelea ili kutwaa tena eneo hilo kutoka kwa waasi.
"Tunawahakikishia jambo moja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haitaruhusu kufedheheshwa au kupondwa. Tutapigana na tutashinda," ameongeza.
Mapigano hayo yamewalazimu takribani watu 500,000 kuondoka kwenye makazi yao, na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu, kwa mujibu wa UN