Alhamisi , 7th Nov , 2024

Viongozi wa Serikali wametakiwa kutoa ushirikiano unapohitajika kwa waandishi wa habari ili kuepusha migogoro baina yao ambayo kuna muda imekuwa ikitokea kwa waandishi wa habari kutoa taarifa hizo bila kuweka upande wao.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania(TRF), Deodatus Balile, kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa nane wa Jukwaa la Wahariri, uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.

“Tunaomba ushirikiano kwa taasisi za Serikali kwa maana wamekuwa wakitukwepa tunapohitaji kufanya balancing ya story zetu, halafu tukizitoa wanasema tumelipwa, kutunyima ushirikiabno haimaanishi habari itakuwa imekufa hapana habari inaweza kuruka bila wao kungea", DEODATUS BALILE-Mwenyekiti TEF.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa misingi na weledi kwa kuzingatia kulinda amani ya Tanzania.

"Tunaomba mfanye kazi kwa kuzingatia maadili, sheria na miiko yenu kwa kuzingatia amani ya nchi yetu, sisi Serikali tupo tayari kupokea ushauri, maoni na mapendekezo yeyote na tupo tayari kuyafanyia kazi", EDWARD MPOGOLO-Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa, amewataka Wahariri kuwa makini kuepuka habari za upotoshaji kuelekea kipindi cha uchaguzi.

"Nchi yetu inaelekea kwenye uchaguzi Novemba 27, 2024 , hiki ni kipindi muhimu  kwa vyombo vya habari kufanya kazi kwa welezdi kwa kuzingatia maadili na sheria, wahariri mna dhamana ya kuifanyia vyema kazi yenu , kwani historia inaonesha nyakati kama hizi za kuelekea uchaguzi kumekuwa na habari nyingi za upotoshaji na changamoto kubwa zaidi inachangiwa zaidi na kukua kwa teknolojia ya habari na mitandao, hivyo nitoe wito kwa wale ambao bado hajawajisajili kujisajili na kufanya kazi kwa weledi na usanifu", NICHOLAUS MKAPA-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari.