Jumanne , 1st Oct , 2024

Watu wawili wameuawa kwa kunyongwa na kamba na kutobolewa macho nyumbani kwao katika eneo la Barabara ya Nne jijini Tanga huku baba mwenye nyumba Alii Mohamed Bagidad (60) naye akiwa hajulikani alipo. 

Watu hao walionyongwa na kutobolewa macho ni Saira Ali Mohammed (50), ambaye ni mama mwenye nyumba pamoja na binti wa kazi aliyetambulika kwa jina moja la Asha (20).

East Africa TV imefika nyumbani kwa marehemu na kuzngumza na majirani wa familia hiyo ambao wamesema walikuta miili miwili ya mama mwenye nyumba na mfanyakazi wake ikiwa na kamba shingoni wakiwa wamewekwa nguo mdomoni. 

"Baada ya jirani mmoja kuja kugonga kwenye hii nyumba na kukuta ukimya alilazimika kuchungulia ndani ndipo akamuona mama mwenye nyumba yupo chini amelala na ikaonekana miguu ya msichana wa kazi lakini yule mama mwenye nyumba alivyokuwa akionekana pale chini alionekana kama amekufa wakasema mbona kama amekufa yule aliyepanda juu akateremka ikabidi atafutwe Mwenyekiti wa serikali za mitaa akasema haiwezekani kuvunja mlango itabidi tuwatafute polisi," amesema jirani

"Polisi walivyokuja ikabidi wavunje mlango wa mbele kuingia ndani akaonekana mama yuko kwenye korido ana kamba shingoni na ameshindiliwa taulo mdomoni wakaendelea mbele kwenda chumbani wakamkuta dada wa kazi naye amelala chini ana mtandio mdomoni na kamba amefungwa shingoni ndipo polisi walipofanya taratibu zao za kutoa ile miili ya marehemu na kuiweka ndani ya gari lakini mpaka sasa hatujui tukio wamefanyiwa na nani na baba mwenye nyumba mpaka saa hizi anatafutwa hajulikani yuko wapi simu zake tangu jana hazipatikani kwahiyo hapa hatujui nani kafanya tukio hilo, " wamesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa wenyeviti Wilaya ya Tanga Bunu Omari Bahero amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na matukio ya kuuawa na kutekwa ili kuifanya jamii kuishi bila hofu kwenye nchi yao. 

Katika taarifa yake Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga Almachius Mchunguzi imesema tukio hilo limetokea Septemba 30 majira ya saa moja usiku. 

Aidha Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mahali popote atakapoonekana baba mwenye nyumba hiyo ili akamatwe na sheria iweze kuchukua mkondo wake.