Jumatatu , 26th Aug , 2024

Kocha wa zamani wa England Mswedish Sven-Goran Eriksson amefariki dunia leo Jumatatu Agosti 26-2024 kutokana na tatizo la saratani ya kongosho kwa mujibu wa familia yake.

(Kocha Sven-Goran Eriksson enzi za uhai wake)

Taarifa iliyotolewa na watoto wa Eriksson, Lina na Johan imesema"Baba yetu Sven-Goran Eriksson amefariki kwa amani katika makazi yake Bjorkefors yaliyopo Sunne Jumatatu ya leo Asubuhi baada ya kupambana kwa muda mrefu na tatizo la saratani lakini sasa mapambano yameisha kwake".

Eriksson aliyekuwa na umri wa miaka 76, aliifundisha timu ya taifa ya England kwa kipindi cha miaka mitano kati ya mwaka 2001 hadi 2006 na kuiwezesha kufika hatua 3 za robo fainali kwenye michuano ya EURO 2004, kombe la Dunia  2002 na 2006.

Sven-Goran Eriksson ameshinda jumla ya makombe 18 huku amefundisha kwenye 10 tofauti Duniani ikiwamo Sweden, Ureno, Italia, England, Mexico, Ivory Coast, Thailand, UAE, China na Ufilipino huku amefundisha klabu 12 zikiwemo Manchester City, Leicester City, Roma pamoja na  Lazio.