Jumatano , 14th Aug , 2024

Afisa Habari wa klabu ya KMC Khalid Chukuchuku amesema wao kama klabu wapo tayari kusikiliza ofa ya Simba SC kama watahitaji kumsajili kiungo wao Awesu Ali Awesu.

(Kiungo Awesu Ally Awesu akiwa mazoezini Simba SC)

Chukuchuku amesema hayo baada ya KMC kushinda kesi ya kimkataba dhidi ya mchezaji wao Awesu Ali Awesu, ambaye aliondoka kwenye kikosi hicho na kujiunga na Simba SC kinyume na taratibu za usajili kwa mchezaji mwenye mkataba.

‘’Mpira wa miguu ni mchezo wa biashara kama watakuja mezani sisi kama klabu tukiridhia ofa yao basi hakuna sababu ya kumzuia mchezaji kwenda kujiunga na klabu ya Simba. Tutakaa tutajadili thamani ya mchezaji mkataba ambao tulikuwa tumempatia, kiasi cha pesa ambacho tulikuwa tumempatia kipindi tunampa mkataba.’’Amesema Msemaji wa KMC Khalid Chukuchuku

Awesu Awesu alijiunga na Simba baada ya kulipa kiasi cha shilingi Milioni 50 ambayo ilikuwa kwenye mkataba wake na KMC. Lakini hakuishirikisha klabu kwenye mchakato huo kitendo ambacho ni kosa kisheria kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja na KMC mpaka Juni 30, 2025.