Nyumba iliyobomolewa na mvua Lindi
Wananchi hao wameomba serikali iwasaidie ili waweze kuishi kwenye makazi salama lakini pia iwasaidie chakula kwani kwa sasa wamekuwa wakilia njaa.
Wakizungumza na EATV wananchi wanasema mvua mfululizo ndio chanzo cha matatizo, kwa sasa hawana makazi na wengi wao wamekuwa wakilala kwenye masalia ya makazi yaliyoharibika ambayo ni hatari huku wengine wakiomba hifadhi kwa ndugu na majirani au hata kulala nje.
“Tumepatwa na maafa makubwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha, kijiji hiki tu kina kaya wastani wa 330, zaidi ya kaya 100 zimeangukiwa na nyumba, katika hao asilimia kama 50 wanaishi kwenye nyumba za kuomba na hizo nyumba zenyewe ni mbovu kwahiyo siku si nyingi aliyeombwa kukaa atatoka na aliyeomba kukaa atatoka” - Thobias Hokororo Mwenyekiti wa kijiji cha Nagaga.
Mvua kubwa hazijaharibu makazi tu kwani hata chakula na vitu vya thamani ambavyo wangeweza kubadilisha kuwa fedha vimekwenda na maji huku mashamba nayo wakilalamika kuwa yamesafishwa hivyo hawajabakiwa na chochote kinachoweza saidia matumbo yao.
Serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mohammed Moyo imeendelea kutoa tahadhari kwa wananchi kutokaa kwenye nyumba zilizobomoka au kuweka nyufa kwani jambo hilo linahatarisha usalama wa maisha yao huku mikakati kama kufanya tathmini ya gharama za maafa, kutoa elimu ya ujenzi bora kwa wakazi wa nachingwea ili kuepusha adha ya nyumba kuharibika nyakati za mvua zikiendelea kutolewa.