Jumapili , 3rd Dec , 2023

Rais Samia ameagiza maadhimisho ya sherehe za uhuru (9 Desemba) yafanyike Kitaifa kwa kuzindua mchakato na kuandikwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 - 2050 na kimkoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo makongamano ya kujadili hatua za maendeleo yaliyofikiwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Hayo yamesemwa leo Desemba 3, 2023 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na maelfu ya wananchi na viongozi wa mikoa na wilaya waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya Bibi Titi Mohammed kwenye viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani. 

"Tarehe 9 Desemba, 2023 ni maadhimisho ya kumbukumbu ya uhuru wa nchi yetu ambapo mwaka huu Taifa letu litaadhimisha miaka 62, Rais Samia ameagiza maadhimisho yafanyike Kitaifa kwa kuzindua mchakato na kuandikwa kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 - 2050 na kimkoa kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo makongamano ya kujadili hatua za maendeleo yaliyofikiwa," amesema Waziri Mkuu

Aidha waziri Mkuu ameongeza "Kila mkoa umeombwa uandae wazee watano maarufu ili waweze kushiriki tukio hilo litakalofanyika Ikulu lakini pia mwaka kesho Muungano wetu utatimiza miaka 60, kwahiyo tunajiandaa na sherehe za miaka 60 ya Muungano ambazo kitaifa zitafanyika Zanzibar,".

Mapema, Waziri Mkuu alikabidhi magari 22 kwa Wakuu wa Mikoa wanne na Halmashauri mbili ikiwa ni uwakilishi wa magari 125 yaliyokwishawasili nchini kati ya magari 528 yaliyoagizwa chini ya Mpango wa Maendeleo wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa gharama ya shilingi bilioni 57.