Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo
Kauli hiyo ameitoa hii leo Juni 8, 2023, wakati akifungua mafunzo ya viongozi makada wa vyama vya Ukombozi Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2023 katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere (MJNLS) Kibaha mkoani Pwani.
"Ukombozi wa mataifa yetu ulishafanyika na mataifa yetu yapo huru, harakati za ukombozi wa mataifa yetu Kusini mwa Afrika zilishaisha, sasa tuna wajibu wa kupambana na ukombozi wa kiuchumi na wa maisha bora ya wananchi tuliopewa dhamana ya kuwaongoza," amesema Chongolo.
Pamoja na mambo mengine Chongolo amewataka vijana kutambua wajibu wa kuiandaa kesho njema haswa kwa nyakati na mazingira ya sasa, ambapo wanatakiwa kujitambua na kubeba dhima ya uongozi unaolenga kuwatumikia watu kwa weledi na uzalendo mkubwa wa hali juu, kwa ajili ya kubadilisha na kuboresha hali za maisha ya watu.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa takribani wiki mbili, yanajumuisha viongozi na makada wa Vyama vya MPLA, SWAPO, FRELIMO, ANC na ZANU PF, CCM pamoja na CPC.