Jumatano , 7th Sep , 2022

Wakulima wa mbogamboga hasa nyanya katika eneo la Ununio Jijini Dar es Salaam wamesema kuwa hivi sasa, wameshindwa kabisa kumuangamiza mdudu mharibifu maarufu ‘Kanitangaze' kwa kutumia viuwatilifu vilivyopo.

Nyanya iliyoathiriwa na mdudu 'Kantangaze'

Wakizungumza na East Africa Radio baadhi ya wakulima hao wamesema kwamba wanatumia pesa nyingi kununua dawa za kuangamiza wadudu waharibifu lakini dawa hizo zimekuwa zikishindwa kuwaangamiza kabisa hali inayosababisha kuteteleka kwa mitaji yao ambayo wengi wao wamedai kuipata kupitia mikopo.

“Sisi ni vijana na hapa tumejiajiri kwa kufanya kilimo cha mbogamboga ambapo tunajipatia kipato, changamoto kubwa kwa sasa ni huyu mdudu anayeitwa Kamtangaze, huyu kamtangaze ni shida. Hasikii dawa ya aina yoyote.... dawa zote zilizoelekezwa kutumika hazina uwezo kabisa hata wa kumzimisha huyu mdudu. Tumetumia dawa kutoka Arusha na Mbeya ambazo ndo kali lakini hakuna kitu. Nyanya zinaharibiwa sana tunaambulia hasara, anashambulia mno majani na animalistic naanza kula nyanya yenyewe. Wataalam wa kilimo watusaidie tunapata hasara sana" Sabius Possian  - Mkulima wa Mbogamboga Ununio Dar es Salaam.
 
Akiwa kwenye bustani za mbogamboga Ununio, Tabia Hemmed ambaye ni mchuuzi wa nyanya na mbogamboga, amesema mdudu huyo si tu anadhorotesha kilimo cha nyanya.... bali anaathiri biashara ya nyanya kwa wachuuzi wanaonunua nyanya shambani hapo na kwenda kuuza maeneo mbalimbali ya Jiji.