Jumamosi , 27th Aug , 2022

Mwaka 2020 Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 katika pato la taifa na ukuaji wake kwa mwaka ulikuwa ni asilimia 6.7 pekee.

Wakati hali ya ukuaji wa sekta hiyo ikiwa chini,wanaofanya kazi hiyo yaani wavuvi na wadau wengine wanasema kunahitajika uwekezaji mkubwa kwa mitaji na vifaa ili kuleta tija.

EATV ilizungumza na Abubakar Kombo Faki ambaye ni mvuvi katika soko la kimataifa la Feri alisema shughuli ya uvuvi kwao ina ugumu kwakuwa wavuvi wengi hawamiliki vyombo, na ikitokea wamekosa samaki unaandikiwa deni,inapotoka posho yako unakatwa.

‘’Tunakabidhiwa chombo na mafuta tunajaziwa yanaweza kuwa lita 100,lakini tunapoenda kuvua tunaweza tusipate chochote ,hapo mmiliki hatuelewi, anachohitaji ipatikane hela ya lita 100 na sisi tupate posho yetu”Alisema Faki.

Akizungumzia suala la mikopo,Faki amesema kwa upande wao wanaofanya uvuvi ndani ya bahari ni tofauti na wale wanaofanya maziwani,hivyo wanaiomba serikali ingewawezesha mikopo ya vyombo vya uvuvi na vifaa vingine ikiwemo mafuta ili uvuvi uwe na tija.

Akizungumzia suala la vifaa vya uvuvi,Mlemwa Chikwabi Samson ambaye ni katibu wa madalali wa samaki  katika soko la Feri amesema wavuvi wangewezesha vifaa vya kisasa na kupatiwa mitaji wangefanya uvuvi wenye tija.

‘’Wavuvi wakiwezeshwa vifaa wangeweza kuvua katika kina kirefu ,kwakuwa huko wanahitajika kuwa na meli au boti kubwa yenye vifaa vya kisasa kwa kuwa samaki katika bahari ya Hindi wako wengi “Alisema Samson

Kwa upande mwingine akizungumzia kuwezeshwa kwa wavuvi kimitaji,Samson amesema fedha inayotolewa kupitia benki na hata serikali kwa vikundi walivyoambiwa wavianzishe ni ndogo.

‘’Serikali ikihitaji kufanya uwekezaji mkubwa katika uvuvi,ije ikutane na kukaa chini kwa vyama na vikundi wa uvuvi ili kuweka mkakati wapamoja katika kuiboresha sekta hii’’Alisema Samson

Danford Namate ambaye ni katibu biashara zone namba 1 Soko la Feri amesema tumejiunga vikundi vingi na tunaiomba serikali kuingilia kati katika kufanikisha uvuvi wenye tija,mfano kwasasa kuna mabadiliko ya hali ya hewa, samaki hawapatikani kiasi kikubwa na wanauzwa bei ya juu.

“Samaki aina ya changu na vibua kwa kipindi hiki cha upepo wanapatikana kwa shida na bei ya samaki changu ni shilingi elfu 12 wakati awali kilo moja ilikuwa elfu sita,hivyo inatuumiza sisi wafanyabiashara.”Amesema Danford Namate -Katibu biashara zone namba 1 Soko la Feri.

Aidha,serikali imesema utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 ulioanza hivi karibuni unalenga kuifanya Sekta ya Uvuvi na ukuzaji viumbe maji kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mpango huo.

Pia kupitia tovuti ya Wizara ya Mifugo na uvuvi imekitaja kiwango cha ukuaji wa sekta ya uchumi bado ni cha chini hasa ikilinganishwa na uwepo wa rasilimali anuai za maji ikiwemo bahari, maziwa makubwa na madogo, mabwawa, mito na ardhi oevu.