Ijumaa , 19th Dec , 2014

Serikali imesema itawataja hadharani watu wote wanaodaiwa kujihusisha na wizi wa dawa zinazonunuliwa na serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ili waweze kutambuliwa na wananchi,

Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Dornald Mmbando

Serikali imesema itawataja hadharani watu wote wanaodaiwa kujihusisha na wizi wa dawa zinazonunuliwa na serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) ili waweze kutambuliwa na wananchi, ambao wamekuwa wakichangia ukosefu wa dawa katika vituo vya afya na hosipitali za serikali hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Dornald Mmbando wakati wa ukaguzi wa kituo cha afya kijiji cha Msoga kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani, ambapo amesema tatizo la dawa limekuwa likiongezeka siku hadi siku kutokana na baadhi ya watendaji na watumishi wa serikali wasio waaminifu.

Dkt Mmbando amesema kuwa, serikali imejipanga kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya magonjwa mapya yanayoibuka na kuitikisa dunia, ambapo amewaomba wananchi kutoa taarifa pale wanapomuona mtu mwenye dalili za ugonjwa wanaoutilia shaka ikiwemo ugonjwa wa Ebola.

Mbunge wa jimbo la Chalinze mheshimiwa Ridhiwani Kikwete amesema kuwa, tatizo la upotevu wa dawa katika zahanati na vituo vya afya katika jimbo la Chalinze mkoani Pwani, ni kubwa kulinganishwa na upatikanaji wa dawa, jambo linalo athiri utoaji wa huduma za afya, na kuleta manung'uniko toka kwa wananchi wanapoenda kupata huduma kwenye vituo vya afya na zahanati katika jimbo la Chalinze.